Ifahamu dawa ya asili ya maumivu ya hedhi

WANAWAKE wengi hupata maumivu ya tumbo wakati wa hedhi au wanapokaribia kupata hedhi. Maumivu haya hutofautiana toka mwanamke mmoja hadi mwingine kutegemeana na afya ya muhusika. Mbali na kuumwa tumbo, wengine hupata maumivu kichwa, msongo wa mawazo (stress), hofu na hasira za hapa na pale, kuvimba sehemu za siri, kukosa usingizi na matiti kujaa. Hali hii hutokea kwa sehemu kubwa kama matokeo ya homoni kutokuwa sawa (Homone imbalance) na hali hii inaweza kukoma ndani ya siku moja baada ya kuanza hedhi. Wengine hutokwa na damu nyingi kuliko kawaida au kukaa katika siku za hedhi kwa kipindi kirefu kuliko kawaida. Kuna sababu nyingi zinazoweza kuchangia hali hii, ikiwamo kuugua kwa muda mrefu, kupatwa na hofu, huzuni, mshtuko na sababu nyingine za kitabibu. Licha ya tatizo hili kutokuwa na dawa maalumu ya kutuliza, wataalmu wa tiba mbadala wanasema kuna tiba za kutuliza tatizo la kuumwa tumbo. TANGAWIZI. Tangawizi ni moja ya dawa nzuri ya asili, pia ni tiba nzuri kwa kutuliza maumivu wakati wa hedhi. Mgonjwa anashauriwa kutengeneza chai ya tangawizi na kunywa kikombe kimoja (robo lita/ ml 250) kutwa mara mbili, mara baada ya chakula cha mchana na baada ya chakula cha usiku. Pia anaweza kuweka mazoea ya kunywa dawa hii kila siku tatu, kabla ya kuanza hedhi na kuendelea hivyo wakati wote anapokuwa kwenye siku. PAPAI. Papai ni miongoni mwa tunda ambalo hutibu maradhi mengi ikiwamo tumbo la hedhi. Watafiti mbalimbali wa masuala ya tiba mbadala wanasema husaidia wasichana wanaopatwa na tatizo la kutoona siku zao pamoja na wenye maumivu makali pindi waanzapo. Ili liwe dawa, unashauriwa kula kila mara tunda hili hasa lile ambalo halijaiva sana lakini tayari limekomaa na rangi ya ukijani iwe haijaondoka yote. Papai huweza haya yote kutokana na sifa yake kuu ya kuweza kulainisha misuli katika njia ya uzazi, hatimaye kuwezesha utokaji wa hedhi kuwa rahisi bila maumivu yoyote. MSHUBIRI (Aloe vera) Hii ni dawa nyingine ya maajabu ya asili ambayo inatibu maradhi mengi mwilini ikiwamo hili la kupunguza au kuondoa kabisa maumivu wakati wa hedhi. Ili iweze kutibu jeli ya Alo vera inapaswa kuchanganywa na pilipili manga ya unga kidogo, ambapo mgonjwa anapaswa kutumia kwa kunywa kijiko kimoja kikubwa mara tatu kwa siku hadi maumivu yatakapoacha. MDALASINI Tengeneza chai kwa kutumia unga wa mdalasini, kunywa kikombe kimoja kutwa mara mbili wakati wote wa siku zako au anza siku mbili kabla, pia unaweza kuweka mazoea ya kuwa hiyo ndiyo chai yako kila mara ili iwe kama kinga. Inashauriwa kutumia asali badala ya sukari kwenye chai ya mdalasini. JUISI YA KAROTI Juisi ya karoti nayo ni nzuri kwa wenye maumivu ya tumbo la hedhi, mgonjwa anatakiwa kunywa glasi moja kutwa mara mbili wakati wote wa siku zake. Vile vile ulaji wa karoti yenyewe husaidia kujenga kinga dhidi ya ugonjwa huu. MCHAICHAI Kama unasumbuliwa na tatizo hili kila mara basi chai iliyowekwa mchaichai husaidia kutibu. Mgonjwa anapaswa kutumia kikombe kimoja kutwa mara mbili kila siku huku ukitumia asali badala ya sukari. Mazoezi madogo madogo ya viungo husaidia kupunguza maumivu ya tumbo, hivyo mgojwa anapaswa kujizoesha kufanya mazoezi mara kwa mara. Pia inashauriwa wanawake kutokula nyama nyekundu na vitu vya sukari pindi wanapokuwa katika siku zao
.

Post a Comment

0 Comments